Monday, July 25, 2016

Mshtakiwa wa Kuiba Milioni 7 kwa dakika Aongezewa Kesi Nyingine



TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) leo inatarajiwa kuwapandisha kizimbani wafanyabiashara wawili akiwemo Mohamed Mustafa Yusufali ‘Choma’ aliyewahi kutajwa kuwa anajipatia Sh milioni saba kwa dakika moja kwa njia za udanganyifu katika mapato ya serikali.

Choma na mfanyabiashara wa Arusha, Samweli Lema, walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam jana saa 9 mchana kwa ajili ya kusomewa mashitaka yanayowakabili, lakini ilishindikana kwa sababu muda ulikuwa umekwisha.

Washtakiwa hao waliondolewa katika viwanja vya mahakama hiyo jioni na kurudishwa mahabusu kwa kutumia magari ya Takukuru, hivyo leo wanatarajiwa kupandishwa kizimbani kwa ajili ya kusomewa mashitaka yao.

Choma atakuwa anakabiliwa na kesi mbili kwa wakati mmoja, kwa kuwa Julai 12 mwaka huu, alifikishwa mahakamani hapo na wenzake wakikabiliwa na mashitaka 199 likiwemo la kuisababisha serikali hasara ya Sh bilioni 15.6.

Awali kesi ya kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 15.6 inayomkabili Choma na wenzake Alloyscius Gonzaga Mandago, Isaack Kasanga, Taherali Sujjauddin Taherali na Mohamed Kabula ilitajwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shahidi.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, hivyo anaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa. 

Aidha, aliiomba Mahakama iwaruhusu kumchukua Choma kwa ajili ya kumhoji kutokana na tuhuma mpya zinazomkabili na kuahidi kumrudisha mahakamani kabla saa za kazi hazijaisha.

Baada ya kueleza hayo, Hakimu Shahidi alimuuliza mshtakiwa huyo kama ana lolote la kusema, alikaa kimya lakini baadaye alidai kuwa ameelewa na atakuwa tayari endapo wakili wake atakuwepo kwenye mahojiano hayo.

Hakimu Shahidi aliruhusu upande wa Jamhuri umchukue mshtakiwa huyo na kuahirisha kesi hiyo hadi Agosti 5, mwaka huu. 

Choma ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Superior Financing Solution Limited kwa mara ya kwanza alifikishwa mahakamani hapo Julai 12, mwaka huu akikabiliwa na mashitaka 199 ya kughushi, kuwasilisha nyaraka za uongo, uhujumu uchumi utakatishaji fedha na kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 15.6.

Katika mashitaka ya kughushi inadaiwa alighushi hati za usajili kuendesha kampuni 15 ikiwemo Festive General Business Limited zimesajiliwa kihalali nchini jambo ambalo si kweli. Aidha, anadaiwa kuwasilisha nyaraka hizo za kughushi kwa Kamishna wa Kodi Ofisi za TRA Mkoa wa Kinondoni ili kuonesha kampuni hizo zimesajiliwa na zinastahili kusajiliwa kama mlipa kodi.

Mbali na mashitaka hayo, washtakiwa wote wanadaiwa kutakatisha fedha, kwa kuficha uhalali, chanzo na mzunguko wa Sh 1,895,885,000 kwa kuzikopesha fedha hizo kwa watu mbalimbali na kupokea marejesho ya mikopo huku wakijua fedha hizo zimetokana na njia zisizo halali za kughushi na kukwepa kodi.


Yusufali anadaiwa kati ya Januari 2008 na Januari mwaka huu, kwa vitendo viovu vya kughushi na kuwasilisha nyaraka za uongo kwa Kamishna wa TRA, ameisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 15.6 ambazo zilitakiwa kulipwa kama Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).

No comments:

Post a Comment